Wanakijiji Karagwe Kunufaika na Kivuko cha Kisasa Ziwa Burigi
Na Lydia Lugakila
Karagwe
Wananchi katika kata za Rugu na Nyakasimbi, pamoja na maeneo jirani katika wilaya ya Karagwe Mkoani Kagera wanatarajia kuondokana na adha ya kuvuka Ziwa Burigi kwa mitumbwi isiyo salama.
Serikali, kupitia Wizara ya Ujenzi, imetangaza mipango ya kuleta kivuko cha kisasa kitakachorahisisha usafiri na kuboresha usalama wa wakazi wa maeneo hayo.
Hayo yamebainika katika kikao cha Baraza la madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe kilichofanyika katika ukumbi wa Angaza Novemba 13,2024.
Waziri wa Ujenzi na Mbunge wa Jimbo la Karagwe, Innosent Bashungwa, ametangaza habari hiyo njema kwa wananchi.
“Kwa muda mrefu wananchi wa kata hizi wamekuwa wakitumia mitumbwi kuvuka ziwa hili ili kufanya shughuli zao za maendeleo" alisema Waziri Bashungwa.
Waziri Bashungwa alisema, Serikali imeona umuhimu wa kuleta kivuko cha kisasa ambacho kitahakikisha usalama na kurahisisha shughuli zao.
Kuvuka kwa mitumbwi kumeonekana kuwa hatarishi, ambapo Wananchi wamekuwa wakihatarisha maisha yao wanapovuka ziwa hilo kwa shughuli mbalimbali kama Biashara, kilimo, na ufugaji.
Naye Diwani wa kata ya Nyakasimbi, Valensi Kasumini, alieleza furaha yake kwa hatua hiyo, akisema, "Hapo awali, wananchi walikuwa wanatumia mitumbwi ambayo haikuwa salama,lakini kivuko cha kisasa kitatusaidia sana na pia kuimarisha shughuli za uzalishaji.”
Aidha Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Karagwe, Wallece Mashanda, alimpongeza Waziri Bashungwa na serikali kwa juhudi hizo.
“Juhudi zinazofanywa na Serikali ni za kupongeza" alisema Mwenyekiti huyo.
Ujio wa kivuko hiki utaleta ahueni kubwa kwa Wananchi wa Karagwe na kukuza maendeleo,” alisema Mashanda.
Kwa ujio wa kivuko hiki cha kisasa, wananchi wa Karagwe wanatarajia kuingia kwenye enzi mpya ya usafiri salama na unaotegemewa katika shughuli zao za kila siku.
Comments
Post a Comment