Utekaji watu sasa wahamia kwa wachungaji, makanisa.

 

Na mwandishi wetu


Licha ya  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dokta. Samia Suluhu Hassan kuonya  Utekaji wa watu, Watoto wakiwemo wanafunzi Mkoani Dar es Salaam, hivi karibuni hali hiyo haijakoma ambapo hivi sasa  imehamia Wilaya ya Muleba Mkoani  Kagera ambapo Wachungaji na Makanisa yao wanatekwa wanapoabudu kanisani.


Kwa Mujibu wa barua ya Malalamiko ya Wachungaji wa Jumuiya Ndogo ya Kanisa la Jumuiya Kuu ya Wabaptist Tanzania (BCT) ya  Juni 19,2024 iliyoelezwa kwa  OCD Muleba, imedai Polisi walihusika kusimamia utekaji huo wakiwa na mitutu ya bunduki.


Gazeti hili limebaini Jumapili Julai 21, 2024 katika Kanisa la  Kabare lililopo Wilayani Muleba watu wapatao 15 walivamia Kanisa hilo na kutaka kumteka Mchungaji na Mwenyekiti wa Makanisa ya Baptist Jumuiya ndogo ya Muleba aitwaye Domisian Kabyemela hata hivyo watekaji walielemewa na baadhi yao akiwemo Adeliki Mutongole, Delius Kashaba, Gozibert Kunkolidi na Denisi Rajabu kuambulia kipigo cha Mbwa koko.


Utekaji huo unatajwa kuwa wa tatu, ambapo Juni 16, 2024 walifanikiwa kuteka Kanisa la Kijiji cha Kihumulo wakisimamiwa na Polisi wawili wenye bunduki mbili wakiwa nje, huku mchungaji Kariath Kashaba akifanikiwa kukimbia baada ya kudhalilishwa, ambapo Makanisa ya Nshamba, Kigando na Igabiro tayari yamekwisha patwa na hali hiyo.


Aidha akizungumza na Mwandishi wa habari hili mchungaji Domisian Kabyemela  wa kanisa la Wabaptist Kabare kata ya Biirabo Wilayani Muleba alisema kitendo hicho kinamnyima usingizi kwani hana amani na hayuko tayari kuyumbishwa na watu au kikundi chenye njaa walioamua kufanya yasiyo mapenzi ya Mungu huku akiiomba Serikali kumtazama kwa kwa jicho la tatu msajili wa Jumuiya za kiraia nchini kuhusu kukomaa kwa  suala hilo lililoendelea kuitesa mioyo ya waumini wake.


Nao baadhi ya waumini hao akiwemo Deus Kabirondo, Annonceath Omesmo, Silidion Adrian, Philmon Martin wamemuomba Rais Samia kuwasaidia katika mgogoro huo uliopo kati ya Kanisa la Wabaptist Tanzania (KWT) na Jumuiya kuu ya Wabaptist Tanzania (BCT) kwani wamekosa amani na Uhuru wa kuabudu ikiwemo kuacha shughuli zao za kiuchumi na kulinda majengo yao yasitekwe na wahalifu hao huku wakilaani kitendo alichofanyiwa Mchungaji huyo na kuwa hawako tayari kuyumbishwa kiimani.


Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera Blasius Chatanda alipotafutwa alikiri kuwepo kwa hali hiyo na kuwaomba wahusika kutumia busara na hekima kwa kutumia vikao kuutatua mgogoro wa kidini kwani hautatuliwi na Polisi na anayeingilia anakosea na kuwataka watumishi hao wa Mungu kutohama kutoka kwenye wajibu wao kwa Mungu na kuingia katika maslahi yao binafsi na Siasa.


Hata hivyo kwa upande wake mkuu wa Wilaya ya Muleba Mkoani Kagera Abel Nyamahanga alipotafutwa alisema yuko safarini.


Kupitia Nyaraka kadhaa (tunazo), Wachungaji wamemtupia lawama DC Nyamahanga kwa kuchukua nafasi ya Msajili wa Jumuiya za Kijamii, akiwa hana majibu ya Nyaraka tata zinazodaiwa ni maagizo ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi zilizosainiwa na Katibu Mkuu, Ally Senga Gugu.


"Mgogoro huu unakwamisha shughuli za kiuchumi, na unatuathiri kwenye uboreshaji wa daftari la wapiga kura, maana unakosa imani na Serikali kwa sababu Wanafanya matukio haya, wanadai ameruhusiwa na Serikali na sisi hatuamini" alisema mmoja wao.


Pamoja na kulaani watekaji hao ambao wengine wametoka Dar es salaam, wamemnyoshea kidole Mkuu wa Kituo cha Polisi waliyemtaja kuwa ni OC-CID Mallya, kwamba yeye, Msajili na Watendaji wa Wizara hiyo wanakwamisha Juhudi za Rais Samia  maana wanawasumbua na Njoo kesho.


Mbali ya Lawama kwa OCD-CID Muleba, wamemtaka OCS wa Nshamba na Askari waliosimamia utekaji wa Mchungaji Kariat wa Kihumulo, kulirejesha Kanisa hilo mikononi mwa Mchungaji huyo kama walivyoliteka ili kuondoa taharuki, liwachukulie hatua watekaji na polisi waliohusika.

Comments

Popular posts from this blog

Takukuru Kagera kuchukua hatua dhidi ya Rushwa kuelekea uchaguzi wa Serikali za mitaa.

CHATANDA AMMWAGIA SIFA SOPHIA MWAKAGENDA