Ijuka Omuka festival kuufufua upya Mkoa wa Kagera.
Na Lydia Lugakila
Bukoba
Tamasha kubwa na la aina yake la utamaduni litakalopambwa na chakula cha kiasili pamoja na wasanii wakubwa lijulikanalo kama IJUKA OMUKA linatarajiwa kuzinduliwa Desemba 18,2024 Mkoani Kagera huku mgeni rasmi akitarajiwa kuwa Naibu Waziri Mkuu wa Tanzania Mhe. Dotto Biteko lengo likiwa ni kufufua Mkoa huo upya.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Desemba 14,2024 Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mhe. Hajjat Fatma Mwassa alisema kuwa Tamasha la IJUKA OMUKA lenye maana ya *kumbuka nyumbani* ni la pili kufanyika Mkoani Kagera baada ya tamasha la kwanza kuwahi kufanyika Mwaka 2023 ikiwa ni kutokana na Mkoa huo kuwahi kusifika sana na baadae ukashuka ndo maana kumeanzishwa matamasha kama hayo ili kuufufua Mkoa huo na kuurudisha upya ikiwemo masuala ya kiuchumi pamoja na kiutamaduni huku vyakula vya asili vya Mkoa huo vikionyeshwa na kuonjwa.
"Mwaka huu tunafanya Tamasha la pili litakalowaunganisha wazawa na waishio ndani na nje ya Mkoa pia nje ya Nchi ambapo Mwaka jana tulifanya Tamasha la kwanza na halikuhusisha watu wengi sana na litakuwa na matukio manne makubwa" alisema Mwassa
Akitaja matukio hayo makubwa yatakayofanyika katika Tamasha hilo Mkuu huyo wa Mkoa alisema kuwa ni pamoja na Desemba 18 majira ya asubuhi kuanza na dua ya kuuombea Mkoa na Taifa kwa ujumla, na baadae kuzindua maonyesho ya biashara yatakayodumu kwa siku kumi, kongamano la Biashara, ambalo litakuwa maalumu kwa wafanyabiashara na watendaji wa Serikali lenye lengo la kuondoa changamoto zote za kibiashara, mashindano ya pikipiki, na maonyesho ya mavazi na mziki wa kizazi kipya.
Alisema kuwa mgeni rasmi atakuwa Naibu Waziri Mkuu na waziri wa nishati Mhe. Dotto Biteko ambaye atashiriki katika kongamano la uwekezaji, Tamasha la utamaduni, na gala dinner huku akiongeza kuwa vumbi litakalotimka Bukoba halikuwahi kushuhudiwa.
Mwassa aliongeza kuwa uhalisia wa mtu wa Kagera utajionyesha ikiwemo aina mbali mbali za mapishi pamoja na vionjo mbali mbali kama supu ya senene na pilau la senene huku akitaja matokeo yaliyopatikana baada ya kuanzishwa kwa tamasha la kwanza kuwa ni pamoja na kuwezesha wafanyabiashara kufungua viwanja ambapo wengine waliomba viwanja kwa ajili ya kujenga kumbi za mikutano pamoja na mashamba na mambo mengine mengi.
Aliwaomba Wananchi Mkoani humo pamoja na vijana kutumia fursa hiyo ya maonyesho ya biashara kutangaza shughuli wanazozifanya.
Aidha alisema kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dokta Samia Suruhu Hassan amekusudia kwa dhati kuinua uchumi wa Mkoa wa Kagera hivyo hawako tayari kumwangusha na ni lazima kuonyesha fursa hiyo kwa kuipokea, kuithamini, na kuitambua huku akiahidi kuwa watafanya kila linalowezekana kuhakikisha uchumi wa Kagera unafufuka upya.
Kilele cha tashama hilo ni Desemba 26 2024 ambapo litapambwa na wasanii wakubwa akiwemo Msanii wa mziki wa mduara Juma Kivurande, Jay Melody, Sabah Muchacho, Msagasumu, Shemela na Bushoke huku likiwa limebeba kauli mbiu isemayo MAKE KAGERA GREAT AGAIN.
Comments
Post a Comment